Jumamosi , 19th Jan , 2019

Ukiitaja nchi ya Zimbabwe wengi wanajua kuwa Robert Mugabe ndiye Rais wa kwanza wa nchi hiyo tangu uhuru mpaka sasa, na ndio maana hata alipoondolewa madarakani, alipewa heshima ya kuwa Baba wa Taifa hilo.

Lakini ukweli ni kwamba Mugabe hakuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo, yeye aliichukua nchi kutoka kwa Canaan Banana, ambaye ndiye Rais wa kwanza wa nchi hiyo baada ya kupata uhuru kutoka kwa Uingereza, mwaka 1980.

Anaitwa Canaan Sodindo Banana , aliyezaliwa Machi 5, 1936 huko Matabele Land, Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe) kwa mama wa kabila la Ndebele na baba wa kabila la Mosotho.

Canaan alipata fursa ya kusoma kwenye shule za wamisionari wakati wa ukoloni, na kubahatika kuwa mtumishi wa kanisa wa dhehebu la Methodist (Methodist minister), na baadaye kuwa mwalimu mkuu mwaka 1963 hadi 1966.

Mwaka 1961 aliteuliwa kuwa Mwenyekliti wa Baraza la Makanisa Bulawayo, nafasi ambayo aliingoza mpaka mwaka 1971. Banana aliendelea na kazi za kanisa mpaka pale alipoamua kuwa miongoni mwa watu wanaopinga utawala wa kikoloni nchini Zimbabwe, mpaka akaja kuwa Makamu wa Rais wa African National Congress, na hatimaye kulazimika kukimbia Rhodesia (Zimbabwe) na kwenda Japan kabla hajahamia Washngton DC nchini Marekani, ambako aliamua kupiga kitabu huko Wesley Theological Seminary.

Baada ya kurudi Zimbabwe mwaka 1975, alifungwa jela mpaka mwaka 1976, mwaka huo akaambatana na Robert Mugabe kwenye mkutano huko Geneva, na kisha mwaka 1979 alihudhuria mkutano huko London ambao ulizaa matunda ya kuipatia uhuru nchi ya Zimbabwe, na yeye kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo.

Banana aliendelea kuongoza Zimbabwe mpaka mwaka 1987 ambapo aliachia madaraka na Mugabe kuchukua nchi, baada ya Mugabe ambaye alikuwa Waziri wake Mkuu kubadilisha mfumo wa Urais wao kutoka 'Ceremonial office' na kuwa “executive”, na pia kushiriki kwa kiasi kikubwa katika Umoja wa nchi za Afrika, sambamba na kuunganisha vyama vikubwa viwili vilivyopigania uhuru vya ZAPU na ZANU, mpaka kuwa chama kimoja cha ZANU-PF ambacho mpaka sasa ndio kimeshika dola ya nchi hiyo.

Mwaka 1997 Banana alishtakiwa kwa makosa ya ulawiti kufuatia tuhuma zilizotolewa wakati wa kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili mlinzi wake, ambaye alimuua afisa mwenzake ambaye alimtania na kumkebehi kuwa 'Mke wa jinsia moja' wa Banana. Kesi iliunganishwa na tuhuma kuwa alitumia madaraka yake vibaya wakati akiwa Rais, kuwalazimisha baadhi ya wanaume kukubali kufanya nao ngono. Ingawa alikataa lakini mahakama ilimkuta na hatia ya makosa saba ya ulawiti, kujaribu kufanya ulawiti na udhalilishaji mnamo mwaka 1998. Alihukumiwa kwenda jela na kutumikia kwa miezi nane tu.

Mwaka 2003 Banana alifariki dunia kwa ugonjwa wa kansa, ambapo Rais wa Zimbabwe wakati huo, Robert Mugabe ndiye aliyetangaza taarifa za kifo hicho kwenye chombo cha habari cha Taifa.

Taarifa zaidi zinasema kuwa kesi ya Banana ilikuwa ni tukio la aibu kwa Robert Mugabe, kwani ilibainika wazi alikuwa akijua, lakini hakufanya lolote kuzuia au kukemea.