Ijumaa , 19th Dec , 2014

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi. Mwantumu Mahiza amesema Sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kuikwamua nchi kutoka katika umaskini.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi. Mwantumu Mahiza

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi. Mwantumu Mahiza ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) iliyoandaliwa kumpongeza kwa kuongoza vema kundi la wafanyabiashara waliokuwa katika msafara wa Rais Jakaya Kikwete nchini China hivi karibuni.

Amesema Viongozi wa serikali kuandamana na wafanyabiashara nje ya nchi ni muhimu, na hivyo ameitaka TPSF kuwapanga kisekta wafanyabishara wanaokuwa katika misafara hiyo, ili kupata manufaa zaidi wao na nchi kwa ujumla.

Wakati wa ziara hiyo Bi. Mahiza ambaye alikuwa mkuu wa mkoa wa Pwani kabla ya kuhamishiwa Lindi, alitia saini mkataba wa ushirikiano baina ya wafanyabiashara wa China na Tanzania.

Mapema akimkaribisha katika hafla hiyo Mwenyekiti wa TPSF Dk. Reginald Mengi alimpongeza mkuu huyo wa mkoa kwa kuwaongoza vizuri wafanyabiashara wakati wa ziara hiyo ya Rais nchini China, na kumkabidhi hati maalum ya shukrani kwa kazi kubwa aliyoifanya.

Aidha Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwepo walizungumzia walichojifunza katika ziara hiyo.