Jumanne , 10th Dec , 2019

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi hapa nchini (TPSF), Godfrey Simbeye, amesema kuwa bado sekta hiyo ilikuwa inamuhitaji Ali Mufuruki kwa kuwa alikuwa bado hajakamilisha ndoto yake ya kuifikisha mbali sekta binafsi ya Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye.

Simbeye ameyabainisha hayo leo Desemba 10, 2019, wakati wa ibada ya kumuaga Ali Mufuruki, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa wao kama sekta binafsi, wamempoteza kiongozi mkubwa ambaye alikuwa bado anaipigania sekta hiyo na kuwataka viongozi kufuata yale mazuri aliyoyaacha mfanyabiashara huyo.

"Ali hajamaliza kitu ambacho alitaka kukifanya kuhusu sekta binafsi hapa Tanzania, tulikuwa tunaongea mengi na alidai kwamba kazi ya kuendeleza TPSF ilikuwa bado haijakamilika, hata viongozi wetu walioko humu ndani tuna safari ndefu na mimi nadhani kitu ambacho tunaweza kukifanya ni kuendeleza yale aliyoyaanza Ali" amesema Godfrey Simbeye Mkurugenzi TPSF.

Mfanyabiashara maarufu ndani na hata nje ya Tanzania, Ali Mufuruki, aliaga Dunia akiwa nchini Afrika Kusini, alikokuwa akipatiwa matibabu na leo Desemba 10, 2019, ameagwa na ndugu, jamaa na marafiki na amezikwa katika makaburi ya Kisutu Jijini Dar es Salaam.