Waliokuwa na kesi ya uhujumu uchumi waachiwa

Alhamisi , 13th Mei , 2021

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu na Mkurugenzi wa Logistiki, Byekwaso Tabura, baada ya aliyekuwa DPP, Biswalo Mganga, kuonesha nia ya kutokuendelea na kesi hiyo.

Aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu.

Maombi hayo yamepokelewa Mahakamani hapo hii leo mei 13, 2021, na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahahakama hiyo Kassian Matembele, ambapo yaliwasilishwa na upande wa Jamhuri ambao ulieleza kuwa aliyekuwa DPP Biswalo Mganga, hana nia ya kuendelea kuwashtaki watuhumiwa hao katika kesi yao ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili.

Katika kesi ya msingi Laurean Bwanakunu na Byekwaso Tabura, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la utakatishaji fedha wa zaidi ya shilingi bilioni 1.6.