Ijumaa , 14th Oct , 2022

Jumla ya watu sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma mkoani Mara, kwa tuhuma za kumuua Mwalimu Said Hamis, katika Kijiji cha Nyasirori wilaya ya Butiama mkoani Mara na kumjeruhi vibaya mdogo wa Mwalimu huyo.

Watuhumiwa wa mauaji ya Mwalimu wakiwa mahakamani

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo Wakili wa Serikali Monica Hokororo, amesema tukio hilo la mauaji limetokea Agosti 26, 2022, baada ya watuhumiwa hao kudaiwa kumvamia Mwalimu huyo wakati anatoka  katika shughuli zake na kisha kumuua na kumpora vitu mbalimbali ikiwemo kompyuta mpakato na simu za mialama ya kifedha .

Wakili huyo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Thomas Masana ,Magesa Chacha ,Tindo Masagati, Mkongwe Marwa, Masham Juma pamoja na Joseph Kawawa.

Wakiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Stanley Mwakyaba, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochcote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na hivyo watuhumiwa wote wamerudishwa rumande hadi Oktoba 24, 2022.