Wazazi wameaswa kujenga utaratibu wa kuwakagua watoto wao hali zao za kimwili pindi wanaporudi kutoka mashuleni ili kuwalinda na vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Diwani wa Kata ya Magaoni Jijini Tanga Mohamed Rajab wakati wa bonanza la tulivu magaoni lililofanyika kwa lengo la kuzuia vitendo vya uhalifu na mambo maovu katika kata hiyo.
Diwani Rajab amesema wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kuwaamini wageni wanaokwenda kuwatembelea majumbani na hatimaye kuwaacha wanalala na watoto wao wakisahau jukumu la ulinzi wa mtoto ni la mzazi pekee.

Aidha Diwani Rajab amesema kuwa baada ya wazazi kuwapeleka watoto wao mashuleni mara nyingi wanajisahau na kuwaachia jukumu la ulezi walimu pekee jambo ambalo limekuwa likisababisha ulinzi duni kwa watoto wao.
"Mzazi umkague mtoto kwanza umkague madaftari yake na hali yake ya kimwili kwasababu sasa hivi kumekuwa dunia sio ile tunayoitegemea sasa ivi hata mtoto wa kiume ukiacha kumkagua maana yake tayari unakaribisha kitu kibaya ndani ya nyumba na baada ya miaka mitano utakuja kushangaa kwanza anaweza kuea mlevi lakini pili anaweza akakutana na watu wakampa ushoga na tatu anaweza kufikia hata hatua ya uchokoraa yaani mtoto wa mtaani, "alisema Diwani Rajab.
Awali akizungumzia maendeleo ya Kata hiyo ya Magaoni Diwani Rajab amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuwakomboa wanamagaoni na mafuriko yaliyokuwa yakiwakumba hususani nyakati za mvua za masika hali iliyokuwa ikiwalazimu kuhama makazi yao na kujihifadhi mashuleni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Wilaya ya Tanga Hamza Bwanga amewataka wakazi wa kata hiyo kumuunga mkono diwani wao ambaye amekuwa akijitolea kwa kila hali ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika kata hiyo.
Bwanga ameahidi kuwaunga mkono wanamagaoni katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo ili kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia suluhu Hassan.
Amesema kuwa wataweka mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba ili kuwabaini wanaofanyia vitendo vya ukatili watoto na endapo kamati ikishindwa kusimamia na kubaini itakuwa imeshindwa kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya sita.


