Jumatatu , 7th Oct , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bravo Lyapembile,awaondoe kazini watumishi watatu wanaokusanya mapato kwenye stendi ya mabasi, ambao wameajiriwa kindugu na wanatuhumiwa kuiba mapato.

Ametoa agizo hilo leo Oktoba 7, 2019, wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Manispaa ya Singida pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Singida na kumtaka aandike barua ya kuwaondosha kazini leo hii na kutaka wapelekwe watu wengine watakaoenda kusimamia mapato vizuri.

Kuna vijana watatu pale stendi ambao mmewaweka kindugu, yupo Kennedy Francis (mtoto wa Mkurugenzi),Selemani Msuwa (ndugu yake Diwani) na Salehe Rajab Kundya (shemeji yake Diwani mwingine). Andika barua leo hii, hawa vijana waondoke kwenye hiyo kazi, na upeleke timu nyingine ya watu waaminifu,” amesema Waziri Mkuu.

Aidha amewaonya watendaji wa Kata wanaohusika kukusanya mapato, wahakikishe kuwa kila wanapokamilisha makusanyo, wanazipeleka fedha hizo benki na kupatiwa risiti.

Katika ziara yake yansiku nne mkoani humo, Waziri Mkuu amesema tabia nyingine ambayo ameikuta katika ziara hiyo ni pamoja na baadhi ya watendaji wa kubadili matumizi ya fedha na kuacha malengo yaliyokusudiwa.