Yanayotarajiwa kwa Idris Sultan leo

Ijumaa , 22nd Mei , 2020

Mwanasheria wa mchekeshaji Idris Sultan, Ben Ishabakaki amesema kuwa huenda leo mteja wake akaachiwa kwa dhamana ama kupelekwa mahakamani, kwa kuwa tayari Polisi wameshamaliza kumfanyia mahojiano.

Mchekeshaji, Idris Sultan.

Ishabakaki ameyabainisha hayo leo Mei 22, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, na kusema kuwa tayari Idris anatuhumiwa kwa kosa la kuidhihaki picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

"Washamtuhumu na kosa ambalo wanadhani ni halisi sasa, ambalo ni kuifanyia dhihaka picha ya Mh Rais Magufuli kupitia mitandao ya kijamii, tuliambiwa na Makao Makuu ya Polisi, kwamba leo saa 5:00 asubuhi baada ya kupitia faili watatoa dhamana, kama siyo kuitoa basi watampeleka mahakamani" amesema Wakili Ishabakaki.

Msanii Idris Sultan anashikiliwa katika kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam, tangu Mei 19, 2020, na anatuhumiwa kwa kosa la kuicheka picha ya Rais Magufuli.