
Luca Modric akiwa na tuzo ya Ballon d'Or
Tuzo hizo ambazo zilifanyika Jijini Paris, Ufaransa, zilishuhudia nyota huyo wa Croatia akiwapiku Cristiano Ronaldo aliyeshika nafasi ya pili na Antoine Griezmann aliyemaliza nafasi ya tatu.
Akizungumza baada ya kushinda tuzo hiyo, Luka Modric amesema, "ni hisia za kipekee, ni furaha kwangu ambayo haielezeki kwa maneno kufikia katika mafanikio haya".
"Kwanza kabisa napenda niwashukuru wachezaji wenzangu, makocha na uongozi wa Real Madrid ukiongozwa na Rais wa klabu, pili niishukuru familia yangu, mke wangu na watoto wangu walionifanya mimi kuwa mtu sahihi kuwa hapa. Ndoto yangu tangu utotoni ni kucheza timu kubwa na kufanikiwa, Ballon d'Or imenipa zaidi ya mafanikio niliyokuwa nayafikiria, ni zaidi ya heshima," ameongeza Modric.
Tuzo zingine zilizotolewa katika usiku huo ni pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa Dunia chini ya miaka 21, kinda wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe akishinda tuzo hiyo akimbwaga mpinzani wake wa karibu, mlinzi wa Liverpool, Trent-Alexander Anold.
Tuzo ya mchezaji bora wa Dunia kwa upande wa wanawake imekwenda kwa mchezaji wa klabu ya Olympique Lyon na timu ya taifa ya Norway, Ada Hegerberg, akiweka historia ya kuwa mchezazji wa kwanza wa kike kushinda tuzo hiyo.
Pia Luka Modric amevunja utawala wa nyota Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ambao wameshinda tuzo hiyo mara 10 kwa pamoja tangu mwaka 2008, huku Lionel Messi akiachwa katika listi ya tatu bora ya tuzo hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006.