Jumatatu , 11th Apr , 2016

Klabu ya Yanga imesema, itatumia michezo miwili ya Ligi iliyopo mbele yao kama maandalizi kwa ajili ya mchezo wa marudiano pamoja na kurekebisha makosa yaliyotokea katika mchezo wa awali wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya nchini Sudan.

Yanga wanashuka dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam jumatano ya Aprili 13 kucheza dhidi ya Mwadui na Aprili 16 dhidi ya Mtibwa Sugar ikiwa ni michezo ya Ligi kuu ya Soka Tanzania bara.

Kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amesema, wameweza kumaliza mchezo wa awali lakini hawakuweza kutimiza malengo waliyojiwekea ya kuweza kupata magoli mengi lakini wanaamini wataweza kupata matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano.

Mwambusi amesema, malengo yao ni kuweza kutetea kombe la Ligi kuu ya Soka Tanzania bara pamoja na klabu bingwa afrika suala ambalo wanaamini litawezekana kwani wanaendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano unaotarajiwa kupigwa Aprili 20 Mwaka huu nchini Misri.