Nugaz awapa ahadi nzito mashabiki wa Yanga

Jumatatu , 1st Jun , 2020

Afisa Mhamasishaji na Msemaji wa klabu ya Yanga, Antonio Nugaz ametoa ahadi nzito kwa mashabiki wa klabu hiyo kuelekea msimu ujao baada ya mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kusainiwa jana.

Antonio Nugaz

Akizungumza baada ya Yanga na mdhamini wake GSM kuingia makubaliano ya kimkataba ya ushauri wa mfumo huo wa mabadiliko na La Liga ya Hispania, Nugaz amesema kuwa amehakikishiwa na bosi wa GSM kuwa klabu itasajili kikosi cha kuvutia na chenye ushindani msimu ujao.

Amesema kikosi hicho kitakuwa na uwezo wa kuchukua ubingwa baada ya mechi 10 msimu ujao kutokana na ubora ambao kitakuwa nacho.

"Nimepokea ujumbe kutoka Afrika Kusini kutoka kwa bwana Ghalib Said Mohamed akisema kuwa atafanya usajili na kuifanya timu iwe ya kuvutia na ya ushindani ili kuhakikisha lengo la msimu 2020/21 ni kuchukua ubingwa kabla ya mechi 10 kumalizika", amesema Nugaz.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendeshaji wa GSM, Hersi Said amesema kuwa watasimamia mfumo mzima wa mabadiliko ya klabu hiyo kuwa ya kisasa, akiahidi kuboresha katika maeneo matatu kuelekea kwenye mabadiliko, ikiwemo taaluma sahihi ya mabadiliko, kutoa ofisi ya kuendeshea mabadiliko hayo pamoja na miundombinu mingine.