Jumanne , 10th Sep , 2019

Nahodha wa Taifa Stars na mshambuliaji wa klabu ya Genk, Mbwana Samatta amezungumzia masuala mengi yanayoihusu Taifa Stars pamoja na klabu yake ya Genk.

Mbwana Samatta

Mahojiano hayo yamefanyika alipokuwa kambini na Taifa Stars katika michezo miwili ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, ambapo pamoja na mambo mengine mengi, Samatta ameonesha kufurahishwa na mbinu za kocha Etienne Ndayiragije, akisema  kuwa zinawasaidia kuwa na ari ya kupambana uwanjani na kuahidi kufanya makubwa chini yake.

Samatta amesema kuwa ndoto kubwa anayoiota kwa sasa ni siku moja kuja kucheza michuano ya Kombe la Dunia, japo hana matumaini ya nchi yake kufikia hatua hiyo kutokana na ugumu uliopo.

Kuhusu kuwepo katika kikosi cha Genk kitakachoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu, ikipangwa na timu vigogo kama Liverpool na Napoli, Samatta amesema kuwa kwake ni jambo kubwa sana kupata nafasi ya kucheza katika uwanja wa klabu ya Liverpool (Anfield) kwakuwa ni klabu kubwa, huku akieleza kuwa binafsi alipendelea angepangwa kundi moja na Barcelona au Real Madrid za Hispania.

"Unaposhiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya huwezi kukosa kukutana na vigogo kama hao, mabingwa wa nchi mbalimbali. Lakini mimi ningependa zaidi ningekutana na Barcelona au Real Madrid, ila hata hivyo Anfield pia ni moja ya sehemu bora sana, si mbaya kucheza na timu kama Liverpool na Napoli ", amesema.

Ikumbukwe kuwa Samatta anakuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, ambapo katika kundi la Genk kuna timu za Liverpool, Napoli na RB Salzburg. Pia atacheza kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Uingereza pindi atakapovaaana na Liverpool katika dimba la Anfield.