Simba kutwaa ubingwa kwa staili ya Liverpool?

Jumamosi , 27th Jun , 2020

Klabu ya Simba SC inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara (VPL) hii leo iwapo Azam FC itashindwa kupata alama tatu dhidi ya Biashara United kwenye mechi itakayopigwa jioni katika uwanja wa Karume mkoani Mara.

Wachezaji wa Simba na Liverpool

Mabingwa hao watetezi wanatarajiwa kucheza kesho dhidi ya Tanzania Prisons huko jijini Mbeya na mechi hiyo ndiyo imepewa nafasi kwa Simba kutwaa ubingwa hata Kama Azama itashinda katika mchezo wa leo.

Azam itaichelewesha Simba kutwaa ubingwa iwapo watashinda, kwani wakikusanya alama zote 21 kwenye mechi 7 zilizosalia watafikisha alama 79 wakati Simba akiwa na alama 78 hadi sasa.

Iwapo Azam ambao kwa sasa wana alama 58 wakafungwa au kupata sare na Biashara United, watakua na uwezo wa kufikisha alama 76 na 77 iwapo tu watashinda mechi 6 za mwisho zitakazosalia baada ya leo ambazo hazitoifikia Simba.

Mahesabu ya Leo ya Simba ni kama ilivyokua kwa Liverpool hapo juzi ambapo ilibidi iombee Chelsea ishinde mbele ya  Man City ambao ndio waliokua na uwezo wa kufikisha alama walizokua nazo, na kuichelewesha kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza. Hatimaye Chelsea ilishinda na Liverpool kutangazwa mabingwa.