Ijumaa , 30th Nov , 2018

Shirikisho la soka nchini TFF limepangua maamuzi yake ya jana ambayo yalikuwa yamebadilisha muda wa mechi zilizopangwa kuchezwa usiku kwenye uwanja wa taifa na kuzirudisha mchana, ikiwa ni baada ya masaa 24 tu kupita.

Wachezaji wa Yanga na JKT Tanzania

Taarifa ya shirikisho hilo iliyotolewa na Afisa Habari wake, Cliford Ndimbo, imebainisha kuwa uamuzi uliotangazwa jana umebadilishwa kutokana na changamoto iliyosababisha usitishwaji wake kutatuliwa.

''Mechi zote za ligi kuu soka Tanzania bara zilizobadilishwa kutoka kuanza saa 12:00 na saa 1:00 jioni na kupelekwa saa 10:00 jioni zitabaki muda huo huo wa usiku na hii ni baada ya kukutana na mmiliki wa uwanja ambaye ametuhakikishia kutatuliwa kwa changamoto hiyo'', imeeleza taarifa ya TFF.

Moja ya mchezo ulioathiriwa na mabadiliko hayo ya ratiba ni ule wa jana kati ya Yanga dhidi ya JKT Tanzania ambao awali ulikuwa uchezwe saa 12 jioni lakini ukarudishwa saa 10:00 jioni.

Mechi zinazochezwa usiku katika uwanja huo ni zile zinazohusisha klabu za Simba na Yanga na huenda zikaongezeka baada ya Azam FC nao kuomba kutumia uwanja huo kwenye mechi zao dhidi ya Simba na Yanga.