Jumapili , 4th Aug , 2019

Kaimu kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Etienne Ndayiragije amesema wamejipanga kuhakikisha kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinafanya vizuri leo dhidi ya wenyeji Kenya katika kuwania kufuzu michuano ya CHAN.

Ndayiragije ametoa kauli hiyo baada ya kikosi cha timu kuwasili nchini Kenya kwa ajili ya kuivaa Harambee Stars baada ya mchezo wa kwanza timu hizo kutoka sare ya bila kufungana Jijini Dar es Salaam.

"Nimeona wachezaji wote wako vizuri kiafya na nimeongea nao, kwa sababu hii mechi tunahitaji kujiandaa kisaikolojia, kwa sababu tunahitaji kutumia nguvu nyingi. Tunaimani maandalizi yameenda vizuri na kila kitu kiko sawa.", amesema Etienne.

Kwa upande wake Rais wa TFF Wallace Karia, amesema wamewatimizia mahitaji yote ya kikosi cha timu ya taifa na wameridhishwa na ushirikiano wa benchi la ufundi na wachezaji, kilichobakia ni  kumuomba Mungu.

Mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam Julai 24 katika Uwanja wa Taifa, Stars ilishindwa kutumia vema uwanja wake wa nyumbani lakini kupitia mchezo wa marudiano bado idadi kubwa ya wapenzi wa soka wanaipa nafasi kubwa Taifa Stars ya kuibuka na ushindi kwenye mnchezo huo.