Jumamosi , 19th Jan , 2019

Nyota wa zamani wa klabu ya Azam FC anayekipiga nchini Hispania katika klabu ya CD Tenerife Shaaban Idd Chilunda, ametolewa kwa mkopo kwenda klabu ya CD Izarra ya nchini humo.

Shaaban Chilunda wa kwanza kulia.

Chilunda ametolewa kwa mkopo ili akapate nafasi ya kucheza zaidi kutokana na kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Tenerife, inayoshiriki ligi daraja la kwanza kwa muundo wa soka la Hispania, daraja ambalo hutoa timu zinazopanda ligi kuu La Liga.

Mkopo wa Chilunda ni wa miezi sita hivyo mfungaji huyo bora wa michuano ya Kagame 2018, ataitumikia klabu hiyo hadi mwisho wa msimu huu kisha kurejea katika kikosi cha Tenerife.

Chilunda akiwa na Club Deportivo Izarra atapata nafasi ya kucheza Segunda Division B, ambayo ni ligi daraja la pili na ya tatu kwenye mfumo wa soka la Uhispania ambayo huipa nafasi timu kupanda Segunda Division na kama itafanya vizuri huko itapanda La Liga.

Segunda Division B inajumuisha timu 80 na zipo kwenyer makundi manne yenye timu 20. Club Deportivo Izarra inashika nafasi ya 14 kati ya timu 20 za kundi la pili.