
Yanga ilianza kujipata bao la kwanza mapema sana ikiwa ni dakika ya tatu ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wake Amis Tambwe akifunga kwa kichwa akimalizia krosi ya winga Simon Msuva.
Yanga iliweza kupata nafasi tatu kupitia kwa Malimi Busungu lakini zote alizipoteza na kupelekea timu kwenda mapumziko Yanga wakiwa wapombele kwa 1-0 tu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko ambapo aliingia Paul Nonga akatoka Malimi Busungu huku Pato Ngonyani akiingia na kutoka Mbutu Twite.
Dakika 57 ya mchezo Thaban Kamusoko aliipatia Yanga bao la pili baada ya kuachia shuti kali akiwa nje ya boksi baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na beki Mwinyi Hajji Mngwali.
Yanga iliendelea kupoteza nafasi baada ya Paul Nonga kuunganishia nje krosi ya Kaseke dakika ya 52, kabla ya Tambwe naye dakika ya 54 kumbabatiza kipa Abrefa Godfrey Yaw shuti lake wakiwa wamebaki wawili wanatazamana.
Tambwe tena dakika ya 71, akaunganishia juu ya lango krosi ya Mwinyi Hajji.
Yanga waliwazidi kimchezo wapinzania wao Cercle ambao nao walipoteza nafasi kadhaa katika mchezo huo ambapo kama washambuliaji wake wangekuwa makini, wangeondoka na ushindi mkubwa zaidi.
Licha ya Cercle de Joachim kuzidiwa mchezo lakini kumekuwa na tofauti pia kwa upande wa wachezaji wa akiba ambapo imezoeleka huwa kunakuwa na wachezaji saba ikiwa ni pamoja na mlinda Mlango wa akiba lakni kwa upande wa wapinzani hawa wa Yanga imekuwa ni tofauti ambapo wachezaji wao wa akiba walikuwa ni watano na hawakuwa na mlinda mlango wa akiba.
Ushindi huo unaipeleka Yanga kwenye hatua ya pili ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika ambapo itakutana na APR ya Rwanda katika hatua inayofuata.
APR ambayo inakutana na Yanga kwenye raundi ijayo ya michuano hiyo, imeshinda mechi yake ya leo kwa magoli 4-1 dhidi ya Mbabane jijini Kigali.
Yanga itaifuata APR jijini Kigali, Rwanda kukipiga mchezo wa kwanza mapema mwezi ujao huku mechi ya marudiano ikipigwa jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kilikuwa: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondani, Vincent Bossou, Mbuyu Twite/Pato Ngonyani dk46, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Malimi Busungu/Paul Nonga dk46 na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya dk78.
Cercle de Joachim: Abrefa Godfrey Yaw, Buckland Jimmy Hendrick/ Laretif Stan dk85, Balisson Paschal Damien, Natrey Isaac, Bazerque Desire, Permal Cedric, Langue Jean Anderson, Rasdarising Bhavish/Maguy Jacque Daniel dk80, Pithiaj Louis Fabien, Odame Abraham na Chiffone Louis Guiyano.