Jumatano , 20th Apr , 2016

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara Yanga hii leo inashuka uwanja wa jeshi wa Borg El Arab kumenyana na Al Ahly nchini Misri katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora.

Katika mchezo huo, Yanga inatakiwa kushinda ugenini au kutoa sare ya mabao kuanzia 2-2 ili kusonga mbele baada ya awali kulazimishwa sare ya 1-1 uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hii inakuwa mara ya tano, Yanga kukutana na Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika, na mara zote nne haikuweza kufanikiwa kusonga mbele kwa waarabu hao.

Mara ya kwanza wababe hao walikutana mwaka 1982 katika Raundi ya Pili na Yanga ikatolewa kwa jumla ya 6-1 ikifungwa 5-0 Cairo na kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es salaam.

Mwaka 1988 zikakutana katika Raundi ya Kwanza na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 4-0 waliyofungwa Cairo baada ya kutoka sare ya 0-0 Dar es salaam.

Mwaka 2009 Yanga wakatolewa kwa jumla ya mabao 4-0 wakifungwa 3-0 Cairo na 1-0 Dar es salaam katika raundi ya kwanza pia.

Yanga ikaandika historia mwaka 2014 ilipowafunga kwa mara ya kwanza Al Ahly Dar es salaam 1-0, bao pekee la nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kabla ya kwenda kufungwa 1-0 mjini Alexandria. Mchezo ukarefushwa hadi dakika 120 kabla ya Ahly kushinda kwa penalti 4-3.

Kwa ujumla, Yanga haijawahi kuitoa timu yoyote ya Kaskazini mwa Afrika kwenye michuano ya Afrika na Al Ahly inakuwa timu pekee ya huko kuwahi kufungwa na mabingwa hao wa Tanzania.