Jumatano , 2nd Mar , 2016

Kocha mkuu wa timu ya Mafunzo Hemed Suleiman Morocco amevitaka vilabu vya soka visiwani humo vibadilike ili vifanye vizuri katika mashindano mbalimbali na kujiondoa katika muonekano wa wasindikizaji katika mashindano ya Afrika.

Kocha Hemed Morocco

Morocco ambaye pia ni kocha mkuu wa Zanzibar Heroes na msaidizi wa Taifa Stars amesema, vilabu hivyo vinatakiwa kujua ni lipi tatizo kwani miaka kadhaa timu za Zanzibar zimekuwa ni wasindikizaji tu katika michuano ya Afrika suala linalofanya kisiwa hicho kuonekana hakina klabu au wachezaji watakaoweza kuitangaza Zanzibar kwa upande wa soka.

Morocco amesema, viongozi wa vilabu wanahitaji kuwa na vitu vingi ikiwemo wachezaji wa kimataifa kwani vilabu vinaposhiriki michezo ya kimataifa lazima wawe na wachezaji wa kimataifa ambao watashirikiana na wachezaji wazawa walio ndani ya klabu kwa ajili ya kucheza kwa malengo na kutimiza malengo waliyojiwekea.

Timu ya Mafunzo ambayo ni wawakilishi wa Zanzibar katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika wamerejea visiwani Zanzibar hii leo wakitokea DR Congo kucheza mchezo wao wa marudiano wa klabu bingwa barani Afrika ambapo walicheza Jumapili na kufungwa bao 1-0, dhidi ya wapinzani wao timu ya AS Vita Club na kufanya watoke kwa jumla ya mabao 4-0.

Katika mchezo wa awali Mafunzo walipigwa 3-0 nyumbani kwao kwenye uwanja wa Amaani mchezo uliochezwa Februari 13 mwaka huu.