Jumatatu , 17th Dec , 2018

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe, amewataka viongozi wa TFF na BMT kukaa chini na kuwapa nafasi wanachama wa Yanga ambao hawakushirikishwa vyema kwenye mchakato wa uchaguzi.

Waziri Harrison Mwakyembe (katikati) na Rais wa TFF Wallace Karia (kulia).

Akiongea leo kwenye mkutano na wana habari jijini Dar es salaam, Mwakyembe amesisitiza kuwa pamoja na wanachama wa Yanga kusikilizwa lakini uchaguzi uko pale pale Januari 13, 2019.

''Msimamo wa Serikali ni Yanga ipate viongozi imara na hata Baraza la Michezo na TFF linatambua hivyo hivyo kwahiyo zoezi liendelee na sisi tumebariki ila tunataka uchaguzi umalizike salama kwa afya ya mpira wa Tanzania'', amesema Mwakyembe.

Kwa upande mwingine Mwakyembe ameeleza kuwa tayari Wizara imefanya kikao cha pamoja na pande zote husika ambazo ni Yanga, BMT na TFF na kujiridhisha kuwa kulikuwa na mapungufu madogo tu hivyo yarekebishwe ili viongozi wapatikane.

Hatua hii imefikiwa baada ya Yanga, kuwasilisha malalamiko yao kwa Waziri juu ya mwenendo wa uchaguzi huo ambao unatarajiwa kuziba nafasi mbalimbali ikiwemo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti.