
Gari la Mo Dewji na baadhi ya maafisa wa usalama wakilikagua. Picha ndogo ni MO Dewji.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali Wankyo Simon, kuomba hati hiyo itolewe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili wa Serikali Wankyo Simon, aliwataja wanaosakwa kuunganishwa na mshtakiwa Mousa Twaleb (46) ni raia wa Msumbiji, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issa Tomo, Zacarious Junior na raia wa Afrika Kusini Phila Tshabalala.
Washtakiwa hao wanatakiwa kuunganishwa katika shtaka la pili na la tatu, ambapo shtaka la kwanza linamkabili Twaleb ambaye, anadaiwa kujihusisha na genge la uhalifu, kati ya Mei mosi mwaka 2018 na Oktoba 2018 katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Johannesburg Afrika ya Kusini.
Katika shtaka la pili inadaiwa ni la kujihusisha na genge la uhalifu ambalo linawahusu washtakiwa wote, shtaka la tatu washtakiwa wote wanadaiwa mnamo Oktoba 11, 2018 katika Hotel Colleseum wilayani Kinondoni, walimteka mfanyabiashara, Mohammed Dewji kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri kinyume cha sheria.
Mshtakiwa Twaleb katika shtaka la nne anadaiwa kutakatisha fedha Shilingi milioni nane, kati ya Julai 10 mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach ambapo alijipatia kiasi hicho cha fedha huku akijua fedha hizo ni mazalia ya genge la uhalifu.
Kesi hiyo imeahirishwa ambapo itatajwa tena Agosti 6 mwaka huu.