
Mrisho Gambo ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Wilaya kinachojengwa eneo la Kontena Njiro, na kusema kwamba mkoa huo hauna hata uwezo wa kulipa watumishi wake kwa pato dogo ulionao, hivyo hakuna mradi unaoweza kutekelzwa na halmashauri yenyewe bila mkono wa Rais Magufuli.
“Asitokee mtu yeyote akawa kifua mbele akisema sisi halmashauri tumefanya hivi, kwa sababu halmashauri haina hata uwezo wa kufanya hivyo kwa sababu haina hata uwezo wa kulipa mishahara, watapata wapi uwezo wa kupeleka miradi ya maendeleo”, amesema Mrisho Gambo.
Mrisho Gambo ameendelea kwa kuwataka uongozi wa halmashauri hiyo kuongeza kasi ya kukusanya fedha, ili waweze kujiongezea kipato cha fedha za maendeleo.
“Lazima muende mkaongeze kasi ya kukusanya fedha kwa ajili ya maendeleo, nasema hivyo kwa sababu mapato ya ndani ya halmashauri ya jiji la Arusha ni bilioni 14 na milioni 500 kwa mwaka, gharama za mishahara ya watumishi peke yake ni bilioni 45, haina hata uwezo ya kulipa watu mishahara, anachokifanya Rais Magufuli anachukua milioni 14. 5 yao, anaongeza na fedha nyingine ili zifike bilioni 43 alipe mishahara, alafu baadaye alete na fedha zingine kwa ajili ya maendeleo”, amesema Mrisho Gambo.