
Vurugu katika maandamano hayo
Mmoja wa viongozi wa muungano huo, Seneta wa Machakos Johnstone Muthama amesema uamuzi wa kuahirisha maandamano hayo umechukuliwa kuipa serikali muda wa kuitisha mazungumzo.
Muungano huo wa 'Coalition for Reforms and Democracy (CORD)' umeipa serikali siku 10 la sivyo urejee maandamano hayo.
Viongozi wa CORD wanataka maafisa wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) wajiuzulu wakisema tume hiyo haiwezi kuandaa uchaguzi mkuu huru na wa haki mwaka ujao.
Walikuwa wameandaa kuandamana hadi ofisi za tume hiyo miji mbalimbali nchini humo hadi maafisa hao wajiuzulu.
Maandamano hayo yamekuwa yakikumbwa na vurugu huku polisi wakishutumiwa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
Jumatatu wiki hii, mmoja wa waandamanaji alifariki kwenye maandamano mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya.
Msemaji wa serikali Eric Kiraithe Jumanne aliambia wanahabari kwamba maafisa 29 wa polisi walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.
Serikali hiyo imesema maandamano hayo ni haramu.
Chanzo: BBC