Tuesday , 2nd Jan , 2018

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekabidhi kadi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa wazee 4000 wa wilaya ya Ruangwa ili waweze kumudu gharama za matibabu bila kulazimika kuwa na fedha taslimu.

Akizungumza na wakazi wa wilaya hiyo, Mh. Majaliwa amesema kwamba anaishukuru Halmashauri ya Wilaya kwa kutenga fedha za kuwalipia wazee matibabu na kuwasisitiza wananchi wa wilaya hiyo kujiunga na na Mfuko wa
Afya ya Jamii.

"Ninatoa wito kwa wananchi wengine walipie sh. 15,000 kwa mwaka ili wapatiwe kadi kwa ajili ya watu sita wa familia zao,  yaani mhusika, mwenza wake na watoto wanne. Bima hii inasaidia kwa vile unapata matibabu hata kama huna fedha taslimu," amesema.

Akitoa ufafanuzi juu ya mpango huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Andrea Chezue amesema mpango wa kutoa kadi za bima ya afya kwa wazee wameuita 'CHF Endelevu' kwa sababu walifanya tathmini na kubaini kuwa matibabu yao yana gharama, na yasipolipiwa, wazee hao hawataweza kupatiwa huduma.

Awali Halmashauri hiyo ilifanya utambuzi wa wazee kuanzia umri wa miaka 60 na kuendelea katika vijiji vyote na kubaini kuna wazee 4000 hivyo kuamua kuwalipia 15000 kwa kila wazee sita ili kuweza kuchangia gharama za matibabu yao.

Halmashauri hiyo imejinasibu kwamba wamepanga kila mwaka, kufanya utambuzi wa wazee katika vijiji vyote ili wale wanaofikisha umri huo (60), nao pia waingizwe kwenye mpango wa Mfuko wa jamii .

Katika sera ya Afya na Sheria ya Utumishi wa Umma inamtaja mzee kuwa ni mtu yeyote aliyefikisha miaka 60 kwa sababu nguvu za kufanya kazi zinakuwa zimepungua.