Friday , 5th Feb , 2016

Timu ya Azam FC imesema itatumia uzoefu walionao pamoja na umakini walioweza kuujenga ugenini kuweza kupambana na kuweza kupata pointi tatu ili kuweza kukaa sawa katika msimamo wa ligi kuu ya soka Tanznaia Bara.

Afisa Habari wa Azam FC Jaffery Iddy Maganga amesema, kikosi kimeingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Mwadui FC utakaochezwa siku ya Jumapili Uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es salaam.

Maganga amesema, Mwadui FC ni timu yenye ushindani na wanawaheshimu kisoka kwani wana ushindani mkubwa tangu mwanzo wa ligi mpaka sasa.

Maganga amesema, watajitahidi kupambana kwani ligi ni ngumu na haina mwenyewe na kwamba unaweza ukafungwa au ukashindwa kutokana na maandalizi yako.

Maganga amesema, mashindano ya mwaliko nchini Zambia yamekisaidia kikosi cha Azam FC kuweza kujiamini na kwa upande wa kocha kuweza kujua mapungufu ya kikosi na kufanyia marekebisho kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya kombe la shirikisho pamoja na muendelezo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara.