Friday , 29th Dec , 2017

Kikosi cha Yanga SC kinatarajiwa kuondoka leo jijini Dar es salaam kuelekea jijini Mwanza kwa ndege maaalum ya kukodi huku ikisafiri bila nyota wake Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu.

Yanga inakwenda kukipiga na Mbao FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu sokaTanzania Bara siku ya Jumapili. Mchezo huo utapigwa kwenye dimba la CCM Kirumba mjini humo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Yanga Dismas Ten amesema klabu itawakosa nyota wake ambao ni vinara wa mabao kwenye timu hiyo, Mzambia Obrey Chirwa mwenye mabao sita ambaye yupo kwao kwa ruhusa maalum.

Mwingine ni Ibrahim Ajibu mwenye mabao matano, yeye ataukosa mchezo huo kwasababu anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano na tayari Yanga imethibitisha kuwa TFF imeshawajulisha kuwa nyota huyo hatakiwi kucheza mchezo huo.

Yanga pia itawakosa nyota wake Thabaan Kamusoko na Kelvin Yondani ambao ni majeruhi wa muda mrefu. Ten pia ameeleza kuwa baada ya mchezo dhidi ya Mbao FC, klabu hiyo itasafiri kuelekea Visiwani Zanzibar kwaajili ya michuano ya Mapinduzi.