Friday , 28th Dec , 2018

Tetesi za nyota wa klabu ya Chelsea na timu ya taifa ya Ubelgiji, Eden Hazard huenda zikatimia miezi michache kutoka sasa baada ya kuhusishwa kwa misimu kadhaa.

Eden Hazard

Nyota huyo amesema kuwa hatma yake ndani ya Stamford Bridge itaamuliwa miezi michache ijayo, msimu wa 2018/19 utakapomalizika.

Akizungumza baada ya kuifikia rekodi ya magoli 100 kwa klabu ya Chelsea kwenye ushindi dhidi ya Watford katika EPL katikati ya wiki hii, amesema, "kwa sasa ninaangalia zaidi muendelezo wangu uwanjani, hatma yangu itajulikana mwisho wa msimu".

"Ninataka kitu kitakachokuwa kizuri kwangu na kwa klabu ambayo imenipa kila kitu. Sitaki kusema 'Ndiyo' kwamba nitasaini mkataba mpya, halafu mwisho wa msimu nisisaini, kwahiyo nitaangalia. Wakati mwingine nikiamka nafikiria kutaka kuondoka, na wakati mwingine nikiamka nafikiria kuendelea kubakia," ameongeza.

Mkataba wa Eden Hazard katika klabu ya Chelsea unamalizika mwaka 2020, ambapo tetesi za kujiunga na mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya, Real Madrid zikizidi kushika kasi hivi sasa, kukiwa na uwezekano wa mchezaji huyo kujiunga nao msimu ujao.

Chelsea inashika nafasi ya nne katika msimamo wa EPL hivi sasa, ikiwa na pointi 40 ambazo ni pointi 11 nyuma ya kinara Liverpool.