Monday , 18th May , 2020

Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Virginia nchini Marekani kimemtunuku shahada ya udaktari mbwa aliyejulikana kwa jina la Moose, akiwa miongoni mwa wanafunzi wengine waliohitimu, katika mahafali iliyofanyika kupitia mtandao.

Mbwa anayejulikana kwa jina la Moore

Mbwa huyo mwenye umri wa miaka 8 alijiunga na chuo hicho mwaka 2014 kama balozi wa uelewa wa masuala ya akili, amekuwa akitumika kwa tiba ya mazoezi katika kitivo cha saikolojia, ambapo amezawadiwa shahada ya udaktari wa wanyama pamoja na wanafunzi wengine.

Sambamba na kazi anazozifanya chuoni hapo ikiwemo kuhudhuria mechi za soka, maonesho ya kumbi za starehe, na utambulisho wa wanafunzi wapya, pia Moore anawasaidia wanafunzi kuyazoea mazingira pamoja na kuwasaidia katika matatizo mengine ya akili, ambapo amewasaidia wanafunzi wapatao 7,500 kwa mujibu wa mmiliki wake, Trent Davis.

"Watu wengi walikuwa hawana uzoefu wa kuishi na watu wengine, au hata na mbwa, kwahiyo kutokana na sababu hizo Moore amewasaidia sana kujihisi salama na furaha", amesema Trent Davis.