Monday , 10th Oct , 2022

Kituo cha Sheria na Haki za Binadam (LHRC) kimeitaka serikali kufuta adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wanaohukumiwa adhabu hiyo kwakuwa ni kinyume na haki ya kuishi.

Wakili Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji LHRC

Ikiwa leo ni maadhimisho ya 20 ya kupinga adhabu ya kifo duniani, Kituo cha Sheria na Haki za Binadam (LHRC) kinaungana na wanachama wengine wa mtandao wa kidunia wa kupinga adhabu ya kifo ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga anatoa wito kwa serikali kuiondoa adhabu hiyo kwani haitoi nafasi kwa mtuhumiwa kujirekebisha tabia. 

“Adhabu ya kifo ni adhabu inayotweza utu wa mtu na kuvunja haki ya kuishi kama ilivyoainishwa katika mikataba ya kimataifa na kikanda ya haki za Binadamu. Pamoja na haki hiyo kuainishwa katika mikataba hiyo, serikali ya Tanzania inatambua adhabu ya kifo katika sheria zake ambapo adhabu ya kifo hutolewa kwa mtu anayetuhumiwa kwa mauaji au uhaini. Ni wakati sasa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuta adhabu ya kifo kwakuwa nchi ni ya Kidemokrasia na inayofuata misingi ya haki za Binadamu.”- Wakili Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji LHRC.

Aidha, baadhi ya raia walioongea na kituo hiki wamedai kuwa wengi wanaohukumiwa kufa kuna uwezekano wakawa siyo wauaji kweli na kwamba inaonekana kuwa ya kisasi zaidi kuliko kuisaidia jamii.

“Kwangu mimi niliwahi kuhukumiwa miaka 30 kwa kosa la kufanya unyang'anyi wa kutumia silaha, nimekaa miaka minne baadaye nikaachiwa na nilihukumiwa miaka 30, na hii maana yake ni kwamba kama ningekuwa natuhumiwa kuua maana yake ni kwamba ningehukumiwa kifo. Hili jambo siyo sawa kibinadamu kwasababu kwanza ni kinyume na haki za binadamu, pili mimi nimekaa sana gerezani na nimewaona watu wengi ambao wamehukumiwa kufa lakini ukweli wakikuelezea siyo wauwaji. Kwahiyo niombe serikali iliangalie hili, hauwezi ukamhulumu mtu kufa, adhabu hailengi kumrekebisha mtu bali ni kumukomoa. Waifanyie marekebisho"- Sadick Bwanga, Mhanga wa hukumu aliyeachiwa huru.