
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Mheshimiwa Majaliwa pia ameagiza viongozi katika mikoa na wilaya kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yote yenye wafugaji na wakulima ambapo pia kuna vyanzo vya maji.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona uharibu wa vyanzo vyote vya maji unadhibitiwa kwa kuwekewa mpango mkakati utakaowezesha kuyatunza maeneo hayo dhidi ya uharibifu wa aina yeyote.
Amesema hayo wakati akiongoza kikao cha pamoja na Mawaziri wa kisekta, Makatibu na Naibu Makatibu wakuu, kamati ya ulinzi na usalama mkoa na wilaya za Morogoro wadau na wasimamizi wa masuala ya ardhi na mifugo ili kutatua, changamoto za usimamizi wa masuala ya ardhi ndani ya mkoa huo.
Kikao hicho kimefuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheahimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Desemba 22, 2022 wakati akifunga njia ya kuchepusha maji na kuanza ujazaji maji kwenye bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP).
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wakuu wa wilaya kuunda kamati za maridhiano baina ya wafugaji na wakulima, ili kutengeneza umoja kati ya makundi hayo mawili,""Wafugaji washirikishwe kuandaa miundombinu ambayo wanyama wao wataitumia kupata malisho, maji pamoja na majosho".
Waziri Mkuu amekubaliana na maombi ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro la kuwaondoa wafugaji walioko katika eneo la mto Kilombero ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.Samia.