Jumanne , 14th Oct , 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa hatua husika za kutekeleza upigaji kura ya maoni ya Katiba iliyopendekezwa zimeanza kuchukuliwa ndani ya serikali na kuwataka wananchi kuwa na subira.

Rais Kikwete ametoa kauli hiyo leo Mkoani Tabora wakati akihutubia taifa katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge zilizoambatana na kumbukumbu ya miaka 15 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Dkt. Kikwete amesema ameipitia vizuri Katiba iliyopendekezwa na kubaini kuwa ni bora na ambayo imezingatia makundi yote ya jamii wakiwemo wanawake wavuvi na vijana, hivyo basi anawaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya maoni wakati ukifika.

Sherehe hizo ambazo pia ni kilele cha wiki ya vijana kitaifa, zimefanyika katika uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mjini Tabora na zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya, wabunge na mawaziri.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete ameelezea umuhimu wa mbio hizo pamoja na chimbuko lake ambapo amesema kuwa Hayat mwalimu Nyerere alianzisha mbio hizo kwa lengo la kudumisha amani, upendo na matumaini na kwamba mbio hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya UKIMWI.

Amesema kuwa Tanzania kwa sasa ina wagonjwa wa UKIMWI Milion 1.4, na maambuki yashuka kutoka asilimia 5.7 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2012, na kwamba maambuki mapya kwa hivi sasa ni takribani Elfu 78.

Rais Kikwete pia ametumia maadhimisho hayo kutoa agizo kwa halmashauri zote nchini kutoa taarifa mara kwa mara kuhusiana na asilimia 10 ya mapato yake inayotakiwa kutengwa kwa ajili ya wanawake na vijana.

Aidha akizungumzia  kudumisha mbio za Mwenge wa Uhuru, Rais Kikwete amesema kuwa, watanzania wataendelea kuwasha na kukimbiza mwenge wa uhuru unaowaangazia hata nchi jirani,  kwani uhuru wa nchi hizo  umepatikana kwa namna moja ama nyingine kutokana na amani iliyopo hapa nchini, kutokana na baadhi ya viongozi wake  kuhifadhiwa hapahapa nchini.

Kauli mbiu ya mbio hizi inasema. KATIBA NI SHERIA KUU YA NCHI, JITOKEZE KUPIGA KURA YA MAONI TUPATE KATIBA MPYA.
Pia Rais Kikwete amewataka vijana wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi disemba pamoja na uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.

Aidha akizungumza kabla ya kukabidhiwa mwenge wa uhuru kutoka kwa wakimbiza Mwenge kitaifa, Waziri wa Habari, Maendeleo ya vijana na Michezo Mh Fenela mkangala amesema kuwa, mwenge wa uhuru umekimbizwa kwa mafanikio ambapo miradi ya maendeleo 1451, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 361, imezinduliwa na nyingine kuwekewa mawe ya msingi.

Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (CHADEMA) kimeitaka serikali kuhakikisha inaboresha daftari la kudumu la wapiga kura kabla ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ili kuwapa fursa watanzania wengi kushiriki kupiga kura katika chaguzi hizo.

Mwenyekiti wa taifa wa Chama hicho, Mhe. Freeman Mbowe ametoa kauli hiyo hii leo jijini Dar es Salaam, wakati chama hicho kilipokutana kikishirikisha kamati kuu ya chama ambapo pamoja na mambo mengine watajadili namna chama hicho kitakavyoshiriki katika chaguzi hizo ama kutoshiriki...