Friday , 18th Nov , 2016

Jeshi la Polisi Tanzania latoa mwezi mmoja kuanzia 21/11/2016 hadi 20/12/2016 kwa wanaomiliki silaha kujitokeza kwa ajili ya uhakiki wa silaha zao.

Kamishna wa Polisi Robert Boaz - Kaimu DCI

 

Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai CP Robert Boaz ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoa tathmini ya zoezi la uhakiki wa silaha lililofanyika mapema mwaka huu.

Kamishna Boaz amesema kuwa katika zoezi lililofanyika kati ya tarehe 22 Machi hadi 30 Juni mwaka huu, ni asilimia 59.18 pekee ya silaha zilizosajiliwa ndiyo zilihakikiwa wakati asilimia 40.82 zikiwa hazijahakikiwa kutokana na wamiliki kutojitokeza.

Amesema serikali huenda kuna sababu za msingi zilizowafanya wamiliki hao kutojitokeza na kutangaza hatua zitakazochukuliwa kwa wamiliki ambao hawatajitokeza katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.

Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kufuta leseni kwa silaha zote ambazo hazitahakikiwa, kuwatangaza kwenye vyombo vya habari wamiliki ambao hawatahakiki silaha zao, pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Aidha Kamishna Boaz amewataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha silaha zao sasa katika vituo vya polisi, au ofisi za serikali za mitaa, na kwamba atakayefanya hivyo hatachukuliwa hatua za kisheria.