Sunday , 16th Apr , 2017

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi Isaac Amani Masawe amesema hali ya ulinzi na usalama kwa watanzania kwa sasa siyo nzuri huku akionesha kukerwa na wanaoshamngilia vifo vya askari 8 waliouawa na majambazi, wilayani Kibiti mkoani Pwani

Askofu Isaac Amani

Askofu Amani ametoa kauli hiyo leo katika Ibada ya Pasaka Kitaifa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme Mjini Moshi, na kuwataka watanzania kubadilika na kutenda yaliyo mema kwa manufaa ya taifa huku akieleza kusikitishwa na hali ilivyo sasa ambapo imefikia hatua ya majambazi kuua askari

"Kila kitu kinaanza na sisi, hivi sasa majambazi baada ya kutuua sisi, majambazi yamefikia hatua ya kuua askari wetu... cha ajabu wapo wananchi wanaosherehekea mauaji hayo, hiyo maana yake ni kwamba yapo makundi miongoni mwetu, wapo wa upande huu na upande ule...Hali siyo nzuri, tunahitaji kutoka hapo" Ameonya askofu Amani.

Katika mahubiri yake, askofu Amani amewaasa watanzania kubadili mienendo yao na kuacha tabia za kufanya mambo yasiyokuwa na faida kama vile ulevi wa pombe na dawa za kulevya, biashara ya binadamu, na kuonya watu ambao hujiingiza kwenye ugaidi, ubakaji, ulawiti n.k huku akibainisha kuwa kuendekeza masuala ya aina hiyo ndiko kunalifanya taifa liyumbe.

Pia amewataka watanzania kutumia elimu yeo kujifunza mambo mazuri na yenye manufaa pamoja na kufuata taratibu za afya ikiwa ni pamoja na kupima afya kila wakati na kutambua umuhimu wa kuwa na kutumia bima za afya.

WANASIASA

Katika hatua nyingine, Askofu Amani amewataka wanansiasa nchini kujali zaidi masuala yenye manufaa kwa taifa badala ya kutumia muda mwingi katika mambo ya kujenga vyama vyao.

"Wanasiasa watumie nguvu kwenye maendeleo ya wananchi kuliko kimarisha vyama vyao, hii nchi siyo ya vyama" Alisema Askofu.

Pamoja na hayo, Askofu Amani amewataka watanzania kujiamini na kutumia rasilimali zao wenyewe kujiletea maendeleo badala ya kutegemea wawekezaji.

"Hatujiamini, hatujitumi, watakuja wawekezaji watutawale, hivihivi, tuliwafukuza wakoloni, lakini sasa tunawarudisha tena" Alimalizia