
Baadhi ya wavuvi wakitumia mbinu ya uvuvi haramu (kushoto), kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Abdallah Ulega.
Abdallah Ulega amesema hayo Jijini Mwanza wakati akiongoza kikao cha kufanya tathmini ya operesheni sangara kitaifa awamu ya tatu kwa mwaka 2018, kanda ya Ziwa Victoria kikao kilichohudhuriwa na maafisa waliohusika katika operesheni hiyo.
Amesema kuwa mapato yameongezeka kuanzia Mwezi Desemba mwaka 2017 hadi Mwezi Novemba mwaka 2018, kutoka Shilingi Milioni 457 hadi Shilingi Bilioni 2.2, ambapo amesema kiasi hicho cha pesa kimeongezeka kutokana na mafanikio ya udhibiti wa mianya ya utoroshaji fedha.
“Mwaka 2017 mpaka tunafunga mwaka mwezi Desemba mrabaha wa serikali kuu kabla ya kufanya operesheni ulikuwa Shilingi Milioni 457, mwaka 2018 hadi Mwezi Novemba mrabaha wa serikali kuu ni Shilingi Bilioni 2.290, kutoka Shilingi Milioni 457 mpaka Shilingi Bilioni 2.290 unaweza kuona kwamba ni ongezeko la zaidi ya asilimia 200, hii maana yake kulikuwa na utoroshaji mkubwa wa fedha ambazo zingeingia katika mfumo mkuu wa serikali.” amesema Mhe. Ulega.
Aidha, katika kikao hicho, Mhe. Ulega amesema kabla ya kuanza kwa operesheni za kudhibiti uvuvi haramu, takwimu zilionesha uwepo wa samaki wachanga zaidi ya asilimia tisini, lakini baada ya operesheni hizo samaki walianza kuongezeka kauli iliyoungwa mkono na wafanyabiashara waliohudhuria kikao hicho ambao walisema samaki wakubwa wameanza kupatikana kwa wingi katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Awali katika kikao hicho, akiwasilisha taarifa ya operesheni sangara kitaifa awamu ya tatu mwaka 2018 katika ukanda wa Ziwa Victoria, Afisa Mfawidhi wa kanda hiyo Bw. Didas Mtambalike alisema tangu kuanza kwa operesheni hiyo tarehe 18 Mwezi Oktoba Mwaka 2018 hadi tarehe Moja Mwezi Desemba Mwaka 2018 Shilingi Bilioni 1.172 zilipatikana kutokana na malipo ya faini walizotozwa waliojihusisha na mtukio ya uvuvi haramu.
Bw. Mtambalike pia alisema zoezi hilo limewezesha vyombo vingi vya uvuvi na biashara za bidhaa za uvuvi kusajiliwa na kupatiwa leseni kutokana na elimu ambayo wavuvi walikuwa wakipatiwa ili kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.
Baadhi ya wadau wa uvuvi ambao walipata nafasi ya kutoa maoni yao katika kikao hicho, walimuomba Naibu Waziri wa Mifugo, kuwepo kwa bei elekezi kwa mazao ya samaki ili wavuvi waweze kuuza samaki kwa bei ya uhakika, pamoja na kulifanyia kazi ombi lao la kuendelea kuvua dagaa kwa kutumia taa zinazotumia mwanga wa jua kutokana na kusitishwa kwa taa hizo kwa shughuliza uvuvi.