
Kushoto ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila.
Miaka 10 iliyopita Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), lilifanya uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa baraza hilo huku John Heche kutoka Tarime na David Kafulila wa Kigoma wakiwa wagombea wa nafasi hiyo.
Katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa Agosti mwaka 2009, mshindi hakupatikana kati ya vijana hao waliokuwa machachari ndani ya chama baada ya John Heche kupinga matokeo dhidi ya mpinzani wake kwa madai kuwa kura zilikuwa zimezidi idadi ya wagombea hali iliyopelekea kufutwa kwa uchaguzi huo.
Hata hivyo David Kafulila ambaye alikuwa Msemaji wa CHADEMA kipindi hicho, aliamua kuhamia Chama cha NCCR Mageuzi baada ya uchaguzi huo kufutwa kwa madai ya kwamba huko anaamini ataendeleza jitihada zake za kuimarisha upinzani Tanzania, huku Heche akibakia kuwa diwani wa kata ya Tarime Mjini.
Mwaka 2011, uchaguzi wa BAVICHA ulifanyika tena ambapo Heche aliibuka mshindi kwa kura 143 sawa na asilimia 53.6 kati ya kura zote 239 zilizopigwa dhidi ya wapinzani wake Aidan Sadick, Bernard Mao, Deogratius Kisandu, Edwin Soko na Masoud Suleman.
Heche alishinda nafasi hiyo ya uenyekiti ambayo awali, ilikuwa ikiongozwa na Kamati ya muda chini ya mbunge wa Ubungo, John Mnyika baada ya uchaguzi wa 2009 kukwama.
Safari ya Kafulila 2010 ikaendelea kwa kupata Ubunge wa Kigoma Kusini ambapo mwaka 2014 alijikuta akipata umaarufu mkubwa kwa kuibua sakata la ufisadi wa Escrow.
Katika uchaguzi Mkuu 2015, Kafulila akiwa NCCR chini ya Mwamvuli wa Ukawa alishindwa kufurukuta dhidi ya Hasna Mwilima wa CCM.
Kwa upande wa John Heche Baada ya kuiongoza BAVICHA, Oktoba 2015 alipata ridhaa ya kugombea ubunge wa Tarime Vijijini na kupata nafasi ya kuingia bungeni.
Leo imetimia miaka 10 tangu kutokea kwa sakata la kuvurugika kwa uchaguzi mkuu wa BAVICHA 2009, uliohusisha mapambano makali baina ya John Heche ambaye sasa ni Mbunge wa Tarime Vijijini (CHADEMA) huku David Kafulila akiwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe baada ya kuteuliwa na Rais John P Magufuli Julai 2018, muda mfupi baada ya kujiunga rasmi na CCM.