Monday , 26th Nov , 2018

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe ameziomba taasisi za serikali, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wizara, ambazo zimeipa kazi Wakala wa Majengo ya Serikali Tanzania (TBA), kuwa na subira kwa kuwa taasisi hiyo inauchache wa wafanyakazi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe.;

Akifafanua Waziri Kamwelwe amesema TBA wanakumbwa na changamoto kubwa ya upungufu wa wafanyakazi, ambapo kwa Tanzania nzima ina wafanyakazi 300 pekee, ambao wanajitoa kwa kufanya kazi kwa bidii, huku idadi ya wafanyakazi wanaotakiwa ni 1700.

Utendaji wa TBA bado unaleta mashaka nchi nzima na nimefanya nao kikao nikabaini wapo wafanyakazi 300 pekee na wanatakiwa angalau 1000 ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, hivyo nashauri pamoja na kusikia malalamiko kila upande taasisi mbalimbali naahidi nitayafanya kazi,” amesema Mhe. Kamwelwe.

Akizungumzia ujenzi wa shule ya sekondari ya wavulana, Mhe. Kamwelwe ameipongeza TBA kwa ujenzi wa shule ya kisasa ya sekondari ya wanaume ya Ihungo iliyoathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka 2016 mkoani Kagera.

Nawapongeza sana kwa kujenga shule nzuri tena kwa gharama nafuu ya Bil. 10.4, ukiangalia wengine walitaka kujenga kwa Bil. 36, hivyo TBA wameokoa fedha nyingi sana za Watanzania na kiwango chao cha kazi ni kizuri,” amesema Mhe. Kamwelwe.

Miongoni mwa majengo ambayo yalijengwa na TBA ni hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es salaam maarufu kama hosteli za Magufuli.