Tuesday , 18th Apr , 2017

Msanii wa hip hop anayesumbua na hit ya 'Hela yangu' King Izzy ' Lord Eyes amefichua siri ya mkoa wa Arusha kutokuwa na waimbaji wa nyimbo laini kuwa ni kwa sababu ya kukosekana kwa 'insipiration ya waimbaji katika mkoa huo.

Lord Eyes

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya EA Radio, Lord Eyes amesema kuwa katika maisha ya muziki wa Arusha vijana wengi waliamini kuwa neno bongo fleva ni tusi hivyo hiyo ilikuwa ikiwapa changamoto vijana waliokuwa na vipaji vya kuimba kubadili gia angani na kuanza kufanya mtindo wa rap.

"Miaka ya 1997 ni kipindi nilichoanza kujiingiza kwenye muziki lakini nilikuwa bado shule kipindi hicho watu wanafanya show kwenye concert za kila Jumapili, lakini kila aliyekuwa anapata nafasi ya kupanda jukwaani anafanya rap. wale waliokuwa wanaimba na wao ilibidi wakaze warap kwa sababu kaka zao wote wanafanya rap. Ukosekanaji wa insipiration ya waimbaji ndiyo imepelekea mkoa wa Arusha kukosa wasanii wengi wanaoimba"- Lord Eyes alifunguka.

Lord Eyes pia ameongeza kuwa ile dhana ya kuona bongo fleva ni matusi kwa sasa imeanza kupotea kwenye mkoa huo ndiyo maana pia wanaweza kushirikiana na wasanii wa RnB na hata wasanii waimbaji chipukizi wameanza kuonesha vipaji vyao.

"Hip hop siyo ugumu wa kukunja sura au uchafu, kwanza ukiwa unafanya hip hop unatakiwa uwe Smart kwa sababu unachokiimba ni maisha. Kwa hiyo hata Arusha tumebadilika hatuoni tabu sana kushiriaka na ndugu zetu wa bongo fleva na hakuna tena yale mambo ya kutengana" - Lord Eyes alimaliza kufunguka yote kwenye Planet Bongo.