Rekodi ambayo Azam FC wanaweza kuivunja leo endapo watachukua ubingwa ni ile ya kuwa bingwa mara nyingi zaidi wa michauno hiyo ambapo mwaka jana waliifikia rekodi ya kutwaa ubingwa mara tatu sawa na Simba, hivyo leo wakitwaa itakuwa ni mara ya nne.
Azam FC pia wanacheza fainali mara mbili mfululizo kwa mara ya pili ambapo mara ya kwanza walifanya hivyo mwaka 2012 na 2013, ambapo mara zote walitwaa ubingwa. Mwaka jana timu hiyo ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Simba hivyo ikitwaa tena leo itaweka historia ya kutwaa mara mbili mfululizo katika vipindi viwili tofauti.
Fainali ya leo ni ya 12 tangu Kombe la Mapinduzi lianzishwe. Kwa upande wa URA wanawania taji lao la pili na endapo watafanikiwa kuchukua watakuwa timu mwalikwa ya kwanza kutwaa mara nyingi zaidi. Walitwaa ubingwa wao wa kwanza mwaka 2016.
Azam FC imetinga fainali baada ya kuifunga Singida United bao 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali wakati URA iliifunga Yanga mabao 5-4 kupitia mikwaju ya Penalti kwenye nusu fainali. Mechi itaanza saa 2:15 leo usiku.


