Thursday , 5th Mar , 2015

Timu ya Tanzania Prisons imemteua Kocha Mbwana Makata kuwa kocha mkuu wa timu hiyo baada ya kukatisha mkataba na aliyekuwa kocha wa timu hiyo David Mwamaja baada ya kuona kikosi hicho kuwa katika nafasi mbaya katika wa Ligi kuu Soka Tanzania Bara.

Akizungumza na East Africa radio, Meneja wa Timu hiyo, Lupyuto Mwanguku amesema, wameamua kuachana na kocha Mwamaja na kuwa na Makata ili kuweza kufanya marekebisho ya matokeo na mwenendo mzima wa timu hiyo ambayo mpaka sasa ipo nafasi ya mwisho ikiwa na Pointi 14.

Mwanguku amesema, Kocha Makata ataanza kazi rasmi katika mechi dhidi ya Stand United itakayochezwa Machi 14 jijini Mbeya, japo jana alikuwa na timu kwa muda mfupi akitoa maelekezo katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons na Jkt Ruvu, Uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam, mchezo uliomalizika kwa kutoa sare ya bila kufungana.

Mwanguku amesema, wanaamini uamuzi wa kuwa na kocha Makata utasaidia timu hiyo kuweza kufika mahali wanapopataka katika msimu huu wa Ligi kuu Soka Tanzania Bara.

Mwanguku amesema, ili kuhakikisha wanabakia katika Msimu wa Ligi kuu msimu ujao wanajitahidi kuboresha benchi la Ufundi ikiwa ni pamoja na kuendelea kufanya maboresho katika kikosi kizima cha Tanzania Prisons.