Monday , 25th Jan , 2021

Rais Sahle -Work Zewde leo amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku moja na kukutana na mwenyeji wake Rais John Magufuli wilayani Chato mkoani Geita.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Sahle-Work Zewde mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Geita leo, Januari 25, 2021 kwa ziara ya kikazi ya siku moja.

Akizungumza katika hafla ya ukaribisho,Mh. Rais John Magufuli amesema nchi ya Ethiopia imepiga hatua katika sekta ya mifugo ikiwa ni nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, huku Tanzania ikiwa ya pili kwa mifugo na bado hatua haijapigwa katika sekta hii.

''Waethiopia wanatengeneza  mabegi, mikanda, viatu na kuuza nje ya nchi yao na bidhaa zao zina soko kubwa barani Ulaya, hivyo nimemuomba Mh. Rais Sahle, tupate wawekezaji  pia na sisi tuende kujifunza kutoka kwao'' amesema Rais Magufuli.

Aidha  Rais Magufuli amesema kwa upande mwingine mazungumzo yao yalilenga katika kuwaachia wafungwa 1789 wa Ethiopia ambao waliingia nchini kinyume cha sheria na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria za nchi, namna ya kupanga mbinu za kuwarudisha nyumbani kwao bila masharti yoyote, maana sisi ni ndugu.

Pia tumezungumza kuhusu ushirikiano zaidi hasa katika masuala ya kiuchumi, pia tumemuomba mh. Rais ashughulikie tupate eneo la kujenga ubalozi nchini Ethiopia na wao nimewakaribisha Dodoma wajenge ubalozi wao.

Kwa upande wake Rais wa Ethiopia Mh.Sahle -Work Zewde amesema amefurahi kutembelea nchini Tanzania na hasa katika eneo ambalo ni chanzo cha mto Nile katika ziwa Victoria, ambapo maji yake wanayatumia  hivyo ameahidi kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

''Tunahitaji ushirikiano imara katika nchi hizi mbili, katika maeneo ya biashara na uwekezaji tukiamini ni lazima Afrika tuwekeze hivyo eneo la mifugo ni eneo la kipaumbele '' amesema Rais Sahle

Pia Rais Sahle amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaachia wafungwa waliokuwa wahamiaji haramu wote 1789 wa Ethiopia, na kuaahidi kuwarudisha nyumbani mara moja na kuondoa mzigo kwa Tanzania.