
Mshambuliaji wa Juventus, Paul Dybala (kushoto) wakipongezana na kocha wake wa Juventus, Andrea Pirlo (kulia).
Nedved amesema “Pirlo ni kocha na atakuwa kocha wa Juventus kwa 100%. Tunamkataba na Pirlo, tulijua kutakuwa na magumu yake”.
Kauli ya kiongozi huyo imeondoa wasiwasi ulitawala kuwa, huenda kocha huyo akaoneshwa mlango wa kutokea baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye ligi kuu Italia 'Serie A' kwa kuwa na alama 55, utofauti wa alama 10 na vinara wa ligi hiyo klabu ya Inter Milan inayonolewa na kocha wa zamani wa kocha huyo na klabu ya Juventus, Antonio Conte.
Juventus pia, iliondolewa kwenye hatua ya mtoano ya 16 na klabu ya FC Porto ya Ureno kwa kufungwa jumla ya mabao 4-3 kwenye michezo miwili ya mtoano, kipigo cha mabao 3-1 ugenini na ushindi wa mabao 2-1 kwenye dimba lake la Allianz Arena nchini Italia.
Mawili hayo yalizua utata juu ya Hatma ya kocha huyo kuondolewa klabuni hapo na nafasi yake kuhusishwa kurejea kwa aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Massimiliano Allegri ambaye yu mapumzikoni kufundisha soka kwa sasa.
Tokea Pirlo atua Juventus tarehe 8 Agosti 2020, ameiongoza kwenye michezo 40 kwenye michuano yote, akipata ushindi kwenye michezo 26, sare 8 na vipigo 6 akiwa na 65% ya ushindi.
Hatma ya Paul Dybala Juventus, Utata mtupu
Kwa Upande mwingine, Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Pavel Nedved amezua utata pia juu ya hatma ya mshambuliaji wao hatari, Paul Dybala kwa kusema kuwa klabu hiyo inatathmini nafasi yake sokoni.
Nedved amesema “tunammiss sana. Sidhani kama ameshacheza hata michezo 10 mwaka huu. Uwepo wake utatuhakikishia mbadala tofauti tofauti kwenye mashambulizi na mabao, vitu ambavyo tunavikosa kwa sasa”.
“Ana mkataba wa mwaka mmoja na sina la kuongeza zaidi ya kile kilichesemwa na Mkurugenzi wa michezo (Juventus), Fabio Paratici na Rais (Juventus), Agnelli walivyosema.
“Lakini ni wazi kwamba Juventus tunatathmini nafasi yake sokoni”.
Eneo la ufinyu wa michezo kwa nyota huyo aliyeibeba Juventus kwenye mabega yake kabla ya ujio wa Cristiano Ronaldo kwenye kikosi cha Juventus, Ni dhahiri kuwa hayupo kwenye mipango ya timu, na kauli ya makamu wa rais kukiri kuangalia nafasi yake sokoni inazidi kuibua utata kama atasalia Juventus.
Tokea kuanza kwa msimu huu, Paul Dybala ameshacheza michezo 16 ya michuano yote, amefunga mabao 3 na kutengeneza mabao 2 pekee.