Thursday , 5th May , 2022

Madiwani wa Halmashauri ya Nsimbo Mkoani Katavi wamesalia katika kikao cha baraza la madiwani baada ya kunusa ubadhilifu wa pesa na kutoa maagizo kwa kamati ya wataalamu wa Halmashauri  hiyo na kushindwa kutekeleza maagizo ipasavyo

Mnyukano mkali wa hoja umetokea mpaka kufikia hatua mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo Halawa Malendeja kumtaka Mkurugenzi wa Nsimbo Mohamed Ramadhani kutokumfundisha kazi au majukumu yake.

"Niwaeleze tu mimi najua kazi yangu na sihitaji mtu yeyote hapa anikumbushe wala kunifundisha kazi kila mtu asimame kwenye nafasi yake hakuna kuficha jambo lolote hapa"  - amesema Halawa Malendeja

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mohamed Ramadhani akawakumbusha madiwani wa Halmashauri hiyo kurejea nyuma na kukumbuka jinsi alivyopambana  na mapato ya halmashauri hiyo kuongezeka.

"Naomba tufuate kanuni afu wewe mwenyekiti wa Halmashauri ni mjumbe wa kamati ya wataalamu umo kwenye kamati, kama kuna tofauti nyingine huko naomba zisiletwe hapa kuvuruga kikao na Mimi nimepambana Sana ili kuhakikisha mapato yameongezeka katika halmashauri hii" - ameeleza Mohamed Ramadhani

Aidha diwani wa kata ya Nsimbo Michael Kasanga amempongeza Mkurugenzi kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato mpaka yameongezeka ila akaonya vikali kuwa kuongezeka makusanyo ya mapato sio kibali cha kuruhusu watu kudokoa fedha.

"Kwanza tushukuru kwa kusimamia halmashauri mpaka mapato yameongezeka lakini kuongezeka mapato sio ruhusa ya watu kuiba fedha ,tumechoka kusubiri,au tuendelee kusubiri Mkuu wa Mkoa au wilaya ndo waje watusaidie hapa, kwanza mwizi hasubiri kanuni, Leo niombe tuvunje kanuni na tuamue juu ya hawa wezi" - amesema diwani huyo  wa kata ya Nsimbo Michael Kasanga