Waziri wa maji Jumaa Aweso amesema hatosita kuwachukulia hatua watendaji wa mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira jijini Tanga (Tanga UWASA) watakaobainika wanakwamisha upatikanaji wa huduma ya maji katika jiji la Tanga na mji wa Muheza jambo lililopekea ukosefu wa maji kwa siku 4 mfululizo
Kufuatia hatua hiyo Waziri Aweso ameiagiza mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira (Tanga uwasa) kumwandalia kikao cha pamoja na madiwani na wenyeviti wa mitaa ili kuelezea utendaji kazi wa mamlaka hiyo huku akiahidi kuwachukulia hatua watendaji wazembe watakaobainika kutowajibika ipasavyo.
Pia Waziri Aweso ameitaka Mamlaka hiyo kutoa taarifa mapema kwa wananchi pale inapotokea changamoto ya kukosekana kwa huduma hiyo ili kuondokana na malalamiko yanayoweza kujitokeza huku akiiagiza bodi ya bonde la mto pangani kufanya ufwatiliaji kwa wote wanaofanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji na hatua kali kuchukuliwa dhidi yao.
Waziri Aweso ametoa magizo hayo mkoani Tanga wakati akikagua hali ya upatikanaji wa maji kufwatia kukosekana huduma hiyo kwa siku nne mfululizo chanzo kikitajwa kuwa ni uchafuzi wa mazingira uliofanywa na wananchi katika chanzo kikuu cha mto Zigi hali iliyopelekea maji kuwa na tope jingi na hivyo kuifanya mamlaka hiyo kusitisha huduma kwa wananchi ili kutatua changamoto hiyo.
Aidha waziri Aweso ameitaka bodi ya mamlaka hiyo kukaa na kujadili namna watakavyoweza kupambana na kutatua changamoto zinazopelekea kukosekana kwa maji akiitaka pia kufanya kikao cha pamoja cha haraka na madiwani na wenyeviti wa mitaa kuwaeleza hali halisi ya utekelezaji wake hii ikilenga hasa kuweka wazi taarifa za kiutendaji zitakazosaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.
Akieleza changamoto iliyopelekea kukosekana kwa huduma ya maji kwa siku kadhaa Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Tanga uwasa Geofrey Hilly amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kufanya shughuli zao katika vyanzo vya maji ikiwemo uchimbaji wa madini katika chanzo kikubwa cha Mto Zigi kinachotegemewa na mamlaka hiyo hali iliyopelekea kuchafuka kwa maji.
Kwa upande wake mkurugenzi wa bonde la mto Pangani Segule Segule amekiri uwepo wa baadhi ya wananchi wanaofanya shughuli zao karibu na vyanzo vya maji licha ya jitihada wanazozifanya akiahidi kupokea na kwenda kutekeleza maagizo ya waziri wa Maji Jumaa Aweso.
Akizungumza katibu wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tanga Suleiman Mzee ameipongeza mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Tanga uwasa kwa jitihada za haraka ilizozifanya kutatua changamoto ya kuchafuka kwa maji hali iliyoleta taharuki kwa wakazi wa jiji la Tanga kwa siku nne mfululizo huku akiwataka wananchi kuendelea kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji vilivyopo.
Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira inazihudumia wilaya za Tanga Pangani pamoja na Muheza ikiwa inazalisha lita zaidi ya 30 za maji kwa siku ambapo sasa inatekeleza mradi unaogharimu shilingi Billion 9.18 ambao mara baada ya kukamilika utaiwezesha Tanga uwasa kuwa na uhakika maji ya kutosha kwa mahitaji ya wananchi.

