Thursday , 9th Feb , 2023

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson, amesema kuwa kama taifa umakini usipokuwepo katika namna na jinsi wabunge wamekuwa wakipewa udaktari wa heshima basi kila mtu ndani ya bunge hilo atakuwa na cheo hicho.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson

Kauli hiyo imekuja kufuatia hoja iliyotolewa na mbunge wa Mlalo, Rashid Abdallah Shangazi aliyeomba mwongozo ili kujua kama udaktari wa heshima ambao wamekuwa wakipewa baadhi ya wabunge unazingatia nini pamoja na kutaka kujua endapo mamlaka za elimu nchini zinazitambua PhD hizo.

"Waheshimiwa wabunge ningependa sana tusikilizane kwenye hoja hii, ni muhimu sana kusikilizana kwa sababu tutafika mahali humu ndani kila mtu atakuwa daktari, ni muhimu sana kusikiliza ili ujue ni kama na wewe ukachukue huko wanakochukua au usiende," amesema Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson

Akitolea ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa PhD, Waziri wa Elimu amesema kuwa ili upate PhD inakubidi usomee na upatikanaji wake ni kutoka katika vyuo vinavyotambulika duniani kote, pia unaweza kuipata PhD kwa kufanya utafiti, na kwamba udaktari wa heshima huwa unatolewa na chuo kinachotambulika kwa mtu husika kulingana na kazi zake alizofanya.