Thursday , 4th May , 2023

Serikali imesema taasisi za uhifadhi nchini zimeendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo kufuatia muundo wa sasa wa Jeshi la Uhifadhi kuziwezesha taasisi hizo kufanya kazi zake vizuri huku kila taasisi ikiwa inasimamiwa na Kamishna wa Uhifadhi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Hayo yamesemwa leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakati akijibu swali la Mbunge wa Malinyi Antipas Mgungusi, aliyetaka kujua lini Jeshi la Uhifadhi litapata Kamishna Jenerali ili kukamilisha muundo wa kijeshi na kuleta muunganiko katika divisheni ya NCAA, TANAPA,TAWA na TFS.

"Taasisi hizi zina majukumu tofauti kwa mfano Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zinaruhusu uvunaji na uwindaji wa kitalii, tofauti na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA)," amesema naibu waziri Masanja 

Amefafanua kuwa endapo kutabainika kuwa na changamoto katika utekelezaji wa mfumo huo, serikali itafanya marejeo ya sheria ya wanyamapori ili kuwezesha kuwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu.