Saturday , 13th May , 2023

Mtoto mwenye umri wa miaka 13 mkazi wa wilaya ya Korogwe kijiji cha Hale mkoani wa Tanga  (jina linahifadhiwa), ametekwa na mtu mmoja  aliyekua kwenye gari nyeupe, baada ya kumwambia ‘toka toka nje unaitwa na baba yako’  na kutokomea nae.

Tukio hilo limejiri jana tarehe 12 Mei 2023  majira ya saa 12 jioni, ambapo msako ulianza mpaka leo alipokutwa eneo la Bagamoyo ya Tanga wakiwa hoi, ambapo alimuomba dereva bajaj ampeleke kwa baba yake huko Hale.

Kwa mujibu wa dada wa mtoto huyo aitwae Lilian Msuya, amesema kwamba mtekaji  huyo mwenye rasta  alimpaka unga unaosadikika kuwa ni dawa za kulevya mdogo wake ambaye amekutwa eneo liitwalo Bagamoyo huko huko Mkoani Tanga.

Kwa sasa mtoto huyo anaendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya yake, ambapo inasemekana anaishiwa nguvu miguuni ikiwemo pia maumivu ya kichwa, hali inayoelezwa huenda alipewa dawa nyingi za kulevya.

Taarifa zaidi zinasema mtoto huyo ana kumbukumbu ya mtu aliyemteka kwamba alikua na rasta na hata akionyeshwa picha yake atamjua.

‘’Tunaogopa isije kuwa amafanyiwa ukatili, maana nasikia kuna tabia ya kuteka watoto wa kiume na kuwalewesha ili kuwafanyia ukatili’’ amesema dada huyo.

Kwa sasa mtoto huyo amepelekwa katika hosptali ya Magunga iliyopo Korogwe mkoani Tanga kwa ajili ya uchunguzi.
Akizungumza na EATV  Kamanda wa polisi Mkoani Tanga Henry Mwaibambe, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba ukweli zaidi utajulikana mara baada ya uchunguzi kufanyika