Hizi ndizo ahadi za Magufuli baada ya kuapishwa

Alhamisi , 5th Nov , 2020

Rais John Magufuli baada ya kuapishwa leo tarehe 5 Novemba katika Viwanja vya Jamhuri, Jijini Dodoma  amepata wasaa wa kuzungumza na halaiki katika hafla hiyo ambapo hotuba yake imejikita katika masuala mbalimbali kama ajira, miradi ya maendeleo pamoja na usimamiaji thabiti wa rasimali.

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli akila kiapo cha Urais kwa muhula wa pili.

Kuapishwa kwake, kuna mfungulia mlango wa kuanza muhula wake wa pili madarakani ambapo katika hotuba yake leo amegusia mambo ambayo kutokana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameahidi kuwa Taifa litashuhudia utekelezaji uliotukuka katika kuwaletea wananchi maendeleo.

''Nitashirikiana nanyi kwa karibu katika kuendeleza jitihada zetu za kujikomboa na kujenga Taifa linalojitegemea na katika hilo tunalenga kukamilisha miradi mikubwa tuliyoianzisha na kuanza kutekeleza mingine mipya, tutaimarisha usimamizi wa rasilimali zetu ikiwemo madini, rasilimali za bahari na majini, misiti na wanyamapori pia tutakuza uchumi, kushughulikia changamoto za umaskini, ukosefu wa ajira  hususani kwa vijana, rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za umma'' amesema Rais Dkt John Magufuli.

Rais Magufuli katika mwendelezo wa hotuba yake ameongeza kuwa ''Napenda niwaahidi kuwa bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, dini, kabila ama rangi nitashirikiana nanyi nyote katika kuhakikisha yote tuliyoyaahidi wakati wa kampeni tunayatekeleza''.

Rais John Magufuli ameapishwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof Ibrahim Juma, hafla hiyo ya kuapisha viongozi wa juu kabisa nchini imehudhuriwa na baadhi ya wakuu kutoka nje ya nchi akiwemo Rais wa Uganda, Umoja wa Comoro na Zimbabwe, Mabalozi kutoka nchi 85, wanadiplomasia, wakuu wa mashirika ya kimataifa, Marais wastaafu, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na Usalama, Wajane wa Marais nchini, viongozi wa dini pia , Mawaziri Wastaafu na wafanyakazi waandamizi wa serikali na sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.