CHADEMA yatoa kauli uteuzi wa wabunge viti maalum

Jumapili , 8th Nov , 2020

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika, amesema chama hicho hakijafanya uteuzi wa wabunge wa Viti Maalum.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika

Mnyika ameeleza hayo leo Jumapili Novemba 8, 2020, wakati akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wafuasi wa chama hicho kupitia ukurasa wake wa Twitter ikiwemo kama chama hicho kimeshateua wabunge wa viti maalum.

''Kamati Kuu Chadema haijafanya uteuzi wa wabunge wa viti maalum mpaka sasa. Hivyo hakuna orodha iliyopelekwa na Katibu Mkuu kwa NEC'', ameandika Mnyika.

Kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge la 12 kinatarajiwa kuanza Novemba 10 mwaka huu kama ilivyotamkwa kwenye tangazo la Rais ambapo katika mkutano huo shughuli sita zitafanyika.

Katibu wa Bunge Stephen Kaigaigai, amesema shughuli ambazo zitafanyika ni kusomwa kwa tangazo la kuitisha Bunge, Uchaguzi wa Spika, Kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, kuthibitisha uteuzi wa waziri mkuu, uchaguzi wa naibu Spika na ufunguzi rasmi wa bunge.