Mwanamke hufanya majukumu mengi kwenye jamii
Ni mama, ni dada,ni binti na mengine mengi. Siku ya wanawake Duniani ni siku ya kusherekea vitu vyote ambavyo ni muhimu kwa wanawake na katika kuadhimisha hii siku kituo cha television cha EATV kiliamua kuanzisha mradi wa kuchangia taulo za kike kwa wasichana wenye uhitaji katika shule za Sekondari za Serikali katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
2019 ni mwaka wa tatu tangu kuanzishwa kwa mradi huu, huku lengo kuu likiwa kumuweka msichana huyu shule bila kukosa sababu tu ameshindwa kununua taulo salama za kujihifadhi.
Kwa mwaka 2019 tunatizamia kuwasitiri takribani wasichana 5000 kwa kuwapatia taulo za mwaka mzima kwa kila mmoja sambamba na kuwapa elimu juu ya hedhi salama.
Taarifa ya Changamoto
Nchini Tanzania msichana hukosa masomo kwa siku 3-5 pindi wanapokuwa katika siku zao za hedhi. Vifaa salama vya wao kujisitiri imekuwa changamoto kupatikana .Namthamini ni mradi wenye lengo la kumsaidia msichana huyu asikose masomo sababu ya ukosefu huo.
Lengo la mradi
Lengo letu kuu ni kumsaidia msichana huyu kwa kumpatia taulo salama na kuhakikisha hakosi tena masomo yake na anafikia ndoto zake.